Tuesday, August 14, 2012

"VYOMBO VYA HABARI VIDHIBITI KAZI CHAFU ZA WASANII"

GODFREY LEBEJO. Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Sanaa wa BASATA 

Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limevitaka vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele katika kudhibiti kazi za Sanaa zisizo na maadili kabla ya kwenda hewani ili kuepuka mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Wito huo umetolewa mapema wiki hii na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Sanaa BASATA Vivian Shalua wakati akiiahirisha programu ya Jukwaa la Sanaa inayofanyika kila wiki kwenye Ukumbi wa BASATA ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa, wakati Baraza limefikia hatua nzuri ya kudhibiti hali hiyo, wadau wakuu katika kumaliza tatizo hili ni wasanii wanaotakiwa kutunga kazi bora na zenye maadili huku vyombo vya habari vikiwa na wajibu wa kuchuja kila kazi ya Sanaa inayopokelewa kabla ya kuirusha hewani.

“Basata imeshaviandikia vyombo vya habari kuvielekeza kuwa na kamati za ndani za kudhibiti maadili kwenye kazi za sanaa kabla ya hazijaenda hewani. Hili ni muhimu sana katika kujenga maadili ya mtanzania” alisisitiza Shalua.

Awali akiwasilisha mada kuhusu Historia ya Muziki nchini na hatua zake mkongwe wa muziki wa dansi nchini John Kitime alisema kuwa, kumekuwa na changamoto mbalimbali miongoni mwa wasanii wa fani hiyo hali inayoufanya usifike mbali.

Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na wasanii kutozingatia sheria ya hakimiliki na hakishiriki iliyopo, kuiga midundo ya muziki kutoka nje hali inayosababisha kutokuwepo kwa muziki wenye utambulisho wa Tanzania kama ilivyo kwa mataifa mengine ya Afrika hususan Afrika Kusini.

“Tatizo kubwa ni wasanii wetu kuiga miziki na hata tamaduni za kigeni, hatuwezi kuandaa kazi za Sanaa kufurahisha wazungu au watu kutoka nje tu, tutapotea” alionya Kitime.

Kwa upande wake Rais wa Shindano la ulimbwende la Utalii (Miss Utalii) Gideon Chipungahelo alisema kuwa, kihistoria wanamuziki wetu ukianza na wakongwe waliopo walijikita katika kuiga miziki ya Zaire hivyo kinachofanywa na wasanii wetu wa sasa ni mwendelezo tu.

“Ni wazi kazi iliyopo sasa ni kuwafanya wasanii kujikita katika utajiri mwingi wa makabila yenye midundo mbalimbali tuliojaaliwa. Hapa ndipo tunapaswa kusisitiza” alishauri Chipungajelo.
 Mdau wa Sanaa na mkongwe wa muziki wa dansi nchini John Kitime (kushoto) akisistiza jambo wakati akiwasilisha mada kuhusu Historia ya Muziki nchini kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Idaya ya Ukuzaji Sanaa BASATA Vivian Shalua na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari Godfrey Mungereza.
Rais wa Shindano la Urembo la Miss Utalii Gideon Chipungahelo naye hakuwa nyuma katika kuchangia juu ya tasnia ya muziki nchini.
 Mzee Kassim Mapili aliwaeleza vijana hali ya tasnia ya muziki ilivyokuwa huko nyuma na mabadiliko yaliyopo sasa

Thursday, August 9, 2012

WASANII TUMIENI FURSA KATIKA FANI ZINGINE


 Katibu Mtendaji wa BASATA Ghonche Materego akiieleza Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997 na jinsi inavyofanya kazi zake hapa nchini kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii. Aliwataka wasanii kuacha kukimbilia sanaa za filamu na muziki pekee kwani kuna sanaa nyingine nyingi.

Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limeeleza kusikitishwa na hali iliyopo sasa ya wasanii kuzipa kisogo Sanaa zingine na kung’ang’ania filamu na muziki pekee hali inayowafanya wengi wao kubaki wakihangaika na kulalama.

Akizungumza wiki hii kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa inayofanyika makao makuu ya Basata, Katibu Mtendaji wa BASATA Ghonche Materego alisema kuwa, ni jambo la kushangaza kuona wasanii wakifunga milango yote katika sekta ya Sanaa na kubaki wakihangaika na madirisha mawili tu ya filamu na muziki.

“Ndugu zangu hebu tujiulize tu, Sanaa ni pana sana na ina fursa nyingi katika kutupa ajira na kuzalisha kipato kwa vijana wengi lakini kwa nini wote tunang’ang’ana na filamu na muziki pekee? Fursa nyingine tunamwachia nani? Alihoji Materego.

Alisema kuwa, tatizo lililopo sasa ni kwa vijana kusukumwa na fedha tu badala ya msukumo wa kisanaa hali ambayo imezifanya Sanaa zingine hususan za maonesho na ufundi kupigwa kumbo kutokana na matunda yake kuhitaji muda mrefu na juhudi.

Kwa mujibu wa Materego, ni wakati sasa wa Wasanii kufungua fursa walizozifunga katika fani nyingine za Sanaa vinginevyo haitawezekana kwa wasanii wote kutegemea milango ya filamu na muziki pekee katika kujiajiri bali fikra tofauti zinahitajika

“Haiwezekani tutegemee filamu na muziki pekee, hatutafika. Ni lazima tugeukie fursa zingine katika Sanaa. Sekta yetu ni pana na ina fursa nyingi sana ambazo zimekaa tu zinatusubili. Sisi ndiyo tutazifanya zipendwe na zituingizie kipato” alisisitiza Materego.

Kuhusu wasanii kujitokeza katika masuala mbalimbali yanayowahusu, Materego alisema, kumekuwa na tatizo ambapo katika makongamano, semina na mikutano mbalimbali wasanii wanayoitwa wamekuwa wakijitokeza kwa uchache au kutokuonekana kabisa.

“Mambo mengi yanajitokeza kuhusu wasanii na sekta ya Sanaa kwa ujumla, wasanii wetu wamekuwa wazito sana kushiriki. Hili nalo ni tatizo ni lazima tubadilike tujitokeze katika mambo yote yanayotuhusu” alieleza Materego.

Awali akiwasilisha mada kuhusu Tasnia ya Ubunifu na Mchango wake katika Ajira nchini, Mkurugenzi wa Idara ya Mfuko na Uwezeshaji kutoka BASATA, Charles Ruyembe alisema kuwa, muda umefika sasa wa somo la Sanaa kuanza kufundishwa mashuleni na kutahiniwa kama masomo mengine kwani kwa sasa ni fani inayoajiri vijana wengi.

    Mkurugenzi wa Idara ya Mfuko na Uwezeshaji kutoka BASATA Charles Ruyembe akifafanua masuala mbalimbali kuhusu Sekta ya Ubunifu na mchango wake katika ajira wakati akiwasilisha mada kwenyeJukwaa la Sanaa wiki hii.

Wadau wa masuala ya sanaa, wakifuatilia kwa makini mjadala katika jukwaa la sanaa, Jumatatu.

Wednesday, April 4, 2012

UPIGAJI KURA TUZO ZA MUZIKI MWISHO APRILI 6

 
Afisa kutoka Kampuni ya uhakiki wa mahesabu ya Innovex, Edna Masalu akieleza juu ya utaratibu wa kupiga kura kwenye tunzo za muziki Tanzania wakati akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki makao makuu ya BASATA. Katikati ni Lloyd Zhungu kutoka Innovex na Mratibu wa Jukwaa hilo, Agnes Kimwaga.

Na Mwandishi Wetu

Zoezi la upigaji kura kwa ajili ya kuwapata washindi wa tuzo za muziki Tanzania kwa mwaka 2012 linatarajia kufikia kikomo wiki hii huku wito ukitolewa kwa wadau wa Sanaa kuendelea kuwachagua wasanii wao.

Akizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii makao makuu ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Afisa kutoka Kampuni ya ukaguzi na uhakiki wa mahesabu ya Innovex ambayo ndiyo yenye jukumu la kuratibu zoezi zima la upigaji kura Edna Masalu alisema kuwa, mchakato wake unaendelea vema na unatazamia kufika kikomo wiki hii.

“Zoezi la upigaji kura lililodumu kwa zaidi ya mwezi mmoja na nusu litafikia mwisho wiki hii Aprili 6, wadau wa muziki wanahamasishwa kuendelea kuwachagua wasanii wenye kazi wanazoona ni bora katika kipindi hiki ili kuwawezesha kushinda” alisema Edna.

Kuhusu umakini kwenye zoezi la kupiga kura, Edna alisema kuwa, Kampuni ya Innovex imebuni njia mbalimbali za upigaji kura ili kuwawezesha wadau wa Sanaa wa kada mbalimbali kuweza kupata fursa ya kupiga kura na kuwa sehemu ya tuzo hizo zenye umaarufu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Alizitaja njia hizo ambazo zinatumika kupiga kura kuwa ni pamoja na ujumbe mfupi wa simu ya mkononi kupitia namba maalum, magazeti, vipeperushi na mitandao ya kompyuta ambapo alisisitiza kwamba, kila mtanzania ana haki ya kupiga kura moja tu kwa kila eneo (category) inayoshindaniwa.

“Hakuna njia yoyote ya upendeleo, kura zinapigwa na kuhesabiwa kwa uwazi kupitia mtandao. Toka Academy imeanza hadi sasa zoezi la upigaji kura kwa watanzania mfumo ni wa wazi na hakuna mwanya wa upendeleo” alisisitiza.

Awali, akiongea kuhusu tuzo hizo, Mratibu kutoka BASATA Angelo Luhala alisema kuwa, wasanii na wadau wa Sanaa wanapaswa kuthamini tunzo hizo kama kitu chao kwani ni kitu kilichobuniwa na watanzania kwa ajili ya kukuza muziki nchini.

“Malengo ya tuzo hizi ni kukuza muziki nchini na kuwapa ari wasanii wabuni kazi zenye ubora. Ni wazi msanii anayepata fursa ya kuwa kwenye moja ya kipengele kinachoshindaniwa ni heshima kubwa” Alisisitiza Luhala.

Tuzo za muziki Tanzania kwa mwaka 2012 zinatarajia kufikia kilele chake Aprili 14 mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mlimani City ambapo wasanii mbalimbali watatambuliwa na kutuzwa.

Mratibu wa Tunzo za Muziki Tanzania kutoka BASATA, Bw. Angelo Luhala akisistiza jambo kuhusu tunzo hizo. Pamoja na mambo mengine alitoa wito kwa watanzania kuziona tunzo hizo kama kitu chao wanachopaswa kujivunia.

Mzee Rashid Masimbi ambaye ni moja ya wadau wanaoheshimika kwenye tasnia ya Sanaa nchini akitoa maelekezo na ufafanuzi kuhusu tuzo za muziki huku wadau wakimsikiliza kwa umakini.

Sunday, August 7, 2011

UZINDUZI WA ARTERIAL NETWORK TANZANIA

Waziri wa Habari, Utamaduni na Utalii wa Serikali ya Mapinduzi ya Zainzibar Mh. Jihad, ndiye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Mtandao wa wasanii wa Arterial Network Tanzania.

 Wajumbe wapya wa ANT kutoka kushoto ni Makamu mwenyekiti Ali Bakari, Katibu Mkuu Hassan Bumbuli, Mjumbe sekta ya Muziki Sauda Simba, Mjumbe sekta ya Habari Sophia Ngalapi, Mjumbe sanaa za maonyesho Godfrey Mngereza na Mjumbe sanaa za ufundi Sharifa Juma.


Waziri Jihad akiwa na wajumbe wa ANT waliomaliza muda wao


Mwenekiti wa ANT akitoa neno la shukurani kwa wajumbe wa Mkutano mkuu mara baada ya uchaguzi.